1. Agenda kubwa ni kutawala dhamiri za watu ili waondoe imani yao kwa Mungu aliye muumbaji na kuiweka kwenye kuhofia Matukio ya kutisha yanayoendelea duniani. Kwa kuwa wengi huogopa athari za matukio haya ni rahisi kuchukua muda mwingi kuyajadili hayo kuliko kumjadili Mungu. Tuchukue tahadhali na hili. Tuwaachie walimwengu wajadili mambo yawahusuyo ili sisi tujadili majukumu tuliyopewa na Mungu. Kama ni matukio ya kiunabii hayo yanatuhusu, lakini kama ni mambo ya kisiasa na majanga yatokanayo na athari za kiulimwengu, Mungu amewaachia viongozi na wataalamu wa ulimwengu.
2. Kauli ya Yesu ya kuwa," Angalieni mtu asiwadanganye... maana watu watawadanganya wengi wakitumia jina langu..", inazidi kutimia kila siku. Kelele zinazochanganya mambo ya kidunia na mambo ya kidini, kwa lengo la kutafuta nguvu ya umoja, hizo sizo za watumishi wa Kristo. Zinafanywa na watu waliovaa mavazi ya mwanakondoo lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. Watumishi wa Kristo hawapaswi kushiriki kelele za aina hii. Waachiwe watu wa kidunia ndio waziendeshe. Hii ni kwa sababu watumishi wa Kristo walipewa ujumbe wao na Kristo mwenyewe. Msikubali kuchanganya na hivyo kudanganywa.
3. Kabla ya marejeo ya Kristo, Yesu aliona kuwa ulimwengu utakuwa ukikimbizana na, "Masumbufu ya maisha haya", sambamba na ulaji na ulevi, kwa mujibu wa Luka 21:34, na kwamba kutokana na kuendekeza haya siku ile itawajia walimwengu ghafla,( Luka 21:36). Vitisho vya kuachishwa kazi na hofu ya kutojua jinsi familia itakavyo kula na kunywa na huduma zingine za kijamii, vitasababisha miongoni mwa waliotegemewa kuwa Watumishi waaminifu wa Kristo, waendekeze dini lakini wakiikana imani ya Yesu. Hili litawafanya wachochee kuwasaliti wenzao walioamua kubakia kuwa waaminifu. Inabidi wale walioamua kuwa waaminifu waandae akili zao kukabiliana na hili, siyo kwa vita vya damu na nyama, au kushtakiana mahakamani, bali kwa kuzivaa silaha za nuru. Ukweli wa Kristo ndizo silaha kiini.
4. Mwonekano wa kupungua kwa wateteaji wa ukweli, jambo ambalo linahusisha baadhi ya watumishi walio katika nafasi za uongozi katika taasisi za kikanisa, tendo linalofanya uadilifu na uaminifu vipungue; hayo yatazidi kuongezeka kila mwaka kadri tunavyosogelea marejeo ya Kristo. Hii ni kwa mujibu wa Math 24:10-13. Uhalisia huu hautakiwi kuwa ndiyo mada kuu ya kujadiliwa makanisani. Hii ni kwa sababu huu ni udhaifu wa kitabia. Tunachotakiwa kujadili makanisani ni KUISHINDANIA IMANI YA INJILI. Ujumbe wa Malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12, ndio utakiwao kusemwa zaidi, kwa lengo la kuwaamsha waliolala na kuwaonya wanaochukua nafasi ya Mungu, pale wanapowalazimisha watu kutenda kinyume cha imani na dhamiri zao. Hivyo kulazimishwa kuchanjwa na mamlaka ya kiserikali, wakati Wataalamu wa Afya wakilipinga hili, ni maandalizi tu ya kuwafanya watu hatimaye walazimishwe kuabudu siku ya Jumapili, iliyowekwa na mamlaka ya mwandamu. Mamlaka haya ya kibinadamu hayatakiwi kutiiwa maana yanapingana na kanuni za utendaji wa Mungu. Mungu halazimishi mtu yeyote kufanya chochote. Ametuokoa kwa kutuelimisha kwa kutupatia muda mrefu wa kumchunguza Alivyo. Mlazimishaji ni lazima awe ni mpinzani wa Mungu kimamlaka.
5. Maisha haya yana mwisho wake. Kama siyo kwa kifo cha kawaida, pengine kutokana na uzee, ni kwa kifo cha ugonjwa au kifo cha kulazimishwa na wapinzani wa unachotetea kuwa ni kweli. Inabidi ieleweke kuwa hata yule anayekulazimisha kufanya kinyume cha imani yako na dhamiri yako, utafika muda naye atakufa. Hivyo ni muhimu kujiandaa kwa marejeo ya Kristo, bila kuogopa vitisho vya kuuawa ambavyo vitalazimika kutokea kabla ya marejeo hayo. Uamuzi utakuwa ni wa mtu binafsi, siyo wa kifamilia au wa kikanisa. Unapoendelea kumwabudu Mungu ukiwa na wenzako, haya hayatakiwi kuondoka akilini mwako. Muda siyo mrefu yataanza kutokea. Ujasiri usio na woga ndio utafanya Mungu akuongezee nguvu za Kuishindania imani ya Injili, bila kuwaogopa adui wa ndani na wa nje; ukiazimia akilini kumsikia Kristo akikwambia kuwa, Yeye aliyapitia mateso hayo, na kila mwanafunzi wake, itambidi ayavumilie kwa kuwa ushindi ni hakika baada ya mateso hayo, ( Wafilipi 1:27-30).
ANGALIZO
Hoja hii msomaji nakushauri usiichukulie kuwa ni ya kawaida. Ujumbe huu utatekelezwa upende au usipende. Mwenye mashaka nao atauelewa pengine ukiwa katikati ya utekelezaji. Ukiupuuzia, utakuwa unaipuuzia Biblia na maagizo yake. Ni muhimu uchukue muda kuupatia kipaumbele katika kuyachunguza yaliyoandikwa. Siyo uzushi ni ukweli utakaodhihirika hivi karibuni.
Muhtasari umefanywa na Mch E. Kasika
Mshauri wa Vijana na Viongozi wao
24/01/2022
T
UPE MAONI YAKO HAPA CHINI



No comments: